Putin hataweza kuhudhuria mkutano wa G8

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, amemwambia rais Obama kwamba hataweza kuhudhuria mkutano wa mataifa manane yaliyostawi zaidi duniani, maarufu kama G-8, utakaofanyika katika eneo la Camp David nchini Marekani baadaye mwezi huu.

Ikulu ya White House imesema kuwa imepata habari kwamba waziri mkuu Dimitry Medvedev atachukuwa nafasi ya rais Putin katika mkutano huo.

Katika taarifa, Washington imesema kuwa bwana Putin hataweza kuhudhuria mkutano huo kwa kuwa anahitaji kukamilisha uteuzi wa baraza lake la mawaziri.

Taarifa hiyo imesema kuwa bwana Obama na bwana Putin watafanya mazungumzo katika mkutano wa G20 nchini Mexico mwezi Juni.