Hakuna dalili ya kupata manusura

Maafisa wa uokoaji nchini Indonesia wamesema kuwa hakuna dalili za kupatikana kwa manusura katika mkasa wa ndege ya Urusi inayokisiwa kuanguka katika eneo la milima wakati wa majaribio ya kupaa angani.

Helikopta ya uokoaji imepata mabaki ya ndege hiyo ya kampuni ya Sukhoi yakiwa yametapakaa katika mlima uliopo kusini mwa mji mkuu Jakarta.

Ndege hiyo ilipaa angani hapo jana jumatano ikiwa na wahudumu wanane pamoja na abiria 40.Miongoni mwa abiria hao walikuwa ni watu walioonyesha nia ya kuinunua pamoja na waandishi wa habari.

Ndege hiyo aina ya Superjet-nambari 100 ndio ya kwanza kutengenezwa nchini Urusi kwa ajili ya matumizi ya kiraia tangu kuvunjika kwa muungano wa Kisovyeti.