Masoko ya fedha yayumba Ulaya

Masoko ya fedha barani ulaya yamefunguliwa leo viwango vyake vikiwa chini, huku sarafu ya euro ikishuka kwa karibu miezi minne . Kama takwimu zinavyoonyesha Uhispania inarejea katika mdororo wa uchumi.

Pato la ndani la taifa hilo limeshuka kwa kiwango cha asilimia sifuri nukta tatu katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka.

Nako Ugiriki ambako mzozo wa kisiasa umeongeza hofu juu ya kuimarika kwa sarafu ya Euro , mkuu wa muungano wa vyama vya mrengo wa kushoto Syriza , Alexis Tsi-pras, ameiambia BBC kuwa mipango ya kubana matumizi inaweza kuangamiza sarafu ya Euro .

Syriza inaongoza katika kura ya maoni kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mwezi ujao .

Waziri mpya wa fedha wa Ufaransa Pierre Moscovici, amesema nchi yake inataka mkataba wa mwaka wa ulaya ufanyiwe marekebisho ili kujumuisha mikakati ya kuinua ukuaji wa uchumi.