Kesi za wakenya ICC kuchelewa

Mwendesha mkuu wa mashtaka katika mahakama ya Kimataifa ya ICC, Luis Moreno Ocampo amesema hatapinga kucheleweshwa kuanza kwa kesi za watuhumiwa wanne kutoka Kenya, wakiwemo wawili wanaowania kiti cha urais wa nchi hiyo, wakituhumiwa kuchochea ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Watuhumiwa hao wanne ni pamoja na naibu waziri mkuu Uhuru Kenyatta na waziri wa zamani wa Elimu ya Juu William Ruto, wanashitakiwa kwa kupanga ghasia zilizosababisha vifo vya watu zaidi ya 1,200.

Wote wamesema hawana hatia kuhusu mashtaka hayo.

Ocampo amewaambia waandihsi wa habari mjini New York kwamba watuhumiwa waliomba kucheleweshwa kusikilizwa kwa kesi zao hadi hapo ICC itakapoamua iwapo wakubaliane na rufaa yao ambayo inasema mahakama hiyo ya uhalifu wa kivita haina uwezo wa kisheria wa kuwashtaki.

Hakuna tarehe maalum iliyopangwa kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.ICC itaamua iwapo ikubaliane na ombi hilo la kuchelewesha kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo au la.