Balozi za kigeni zikome kuchapisha ripoti

Afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Uchina, ametoa wito kwa ubalozi za nchi za kigeni mjini Beijing, kukoma kuchapisha ripoti zao kuhusu uchafuzi wa mazingira.

Matamshi hayo ya naibu waziri wa mazingira, yameonekana kulenga ubalozi wa Marekani, ambao huchapisha takwimu zake kuhusu viwango vya uchafuzi wa mazingira ambao ni wa juu sana mjini humo.

Amesema kitendo hicho cha ubalozi wa Marekani kinakiuka maadili na sheria za kimataifa za kibalozi.

Wakaazi wa mji huo wamehoji takwimu hizo, ambazo hadi kufikia mwaka huu hazikuwa zimejumuisha chembechembe zinazodhuru.

Lakini marekani imesema takwimu zake hazipaswi kutegemewa kwa kuwa inatumia kifaa kimoja tu kupima viwango hivyo vya uchafuzi wa mazingira.