Kashfa ya mafuta Nigeria

Polisi nchini Nigeria wamekuwa wakimhoji mbunge mmoja ambaye hivi maajuzi aliongoza uchunguzi wa ripoti iliyoelezea kuwa serikali ya taifa hilo ilipoteza mabilioni ya dola katika ufisadi uliohusisha ruzuku za mafuta.

Mbunge huyo kwa jina Farouk Lawan anashtumiwa kwa kudai dola milioni tatu kutoka kwa kampuni moja ya mafuta ili kuondoa jina la kampuni hiyo kutoka kwa ripoti ya uchunguzi huo wa bunge.

Bwana Lawan amekana madai hayo ya ufisadi huku bunge la Nigeria likikutana hii leo kujadili mstakabali wa mbunge huyo.

Mwandishi wa BBC mjini Lagos, anasema kuwa watu wengi Nigeria wanahoji ikiwa watawahi kujua ukweli ikiwa mbunge huyo alikula rushwa au ikiwa yeye ni mwathirika tu kamapeini chafu ya kumharibia sifa hususan baada ya kufanya uchunguzi ulioonyesha kuwa ufisadi ulifanyika.