Mapigano yaendelea Damascus Syria

Mapigano yameendelea jijini Damascus nchini Syria kufuatia shambulio la bomu lililowaua maafisa watatu wa usalama wa rais Assad siku ya Jumatano.

Serikali na wapinzani kwa pamoja wamesema, idadi kubwa ya watu wameuawa. Vikundi vya upinzani vimesema makombora na helikopta zilitumika katika kile walichokiita ushambuliaji mkubwa wa mabomu kuwahi kuikumba Damascus hadi sasa.

Wapinzani wanaripoti pia kuwa tukio la mazishi yaliyokuwa yakifanyika katika eneo la Sayeda Zeinab kusini mwa Damascus, lilishambuliwa na roketi lililorushwa kutoka ndani ya helikopta na kuua watu wasiopungua sitini.

Kuna ripoti kuwa makombora zaidi yamekuwa yakielekea mjii mkuu wa Damascus. Jeshi la upinzani la Free Syrian army limesema lilihusika katika shambulio lililomuua shemeji wa rais Assad na Waziri wa Ulinzi pamoja na Jenerali wa jeshi la serikali.