Nigeria kuzikamata meli zinazoiba mafuta

Nigeria itazikamata meli za mafuta za magendo katika bahari kuu na kwenye bandari za kigeni kuzuia kupoteza dola bilioni tano kwa mwaka kupitia wizi wa mafuta nchini humo.

Waziri wa Viwanda na Biashara Olusegun Aganga, alisema wanatarajia hatua hiyo kuanza siku chache zijazo. Nigeria kwa miaka arobaini imekuwa ikisumbuliwa na wizi mkubwa wa mafuta yake.

Wizi huo ujulikanao kama usafirishaji kupitia mahandaki unafanyika kwa njia ya mabomba ya mafuta.

Mafuta hayo yanachukuliwa na meli zinazosubiri ufukweni.

Baadaye mafuta hayo yanasafirishwa kwenye masoko ya kimataifa na kuuzwa huko. Sasa waziri wa Nigeria anayeshughulikia viwanda na biashara Olusegun Aganga, anasema Rais Goodluck Jonathan ametoa amri jeshi na vyombo vingine vvya serikali kutumia teknolojia ya setilaiti kufuatilia na kuzinasa meli hizo kokote usafirishaji huo unakopelekwa.