Mwanadiplomasia Syria ajiuzulu London

Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema mwanadiplomasia mwandamizi wa Syria ambaye amekuwa akifanya kazi mjini London amejiuzulu.

Katika taarifa yake, Wizara ya mambo ya nje ilisema Afisa huyo mwandamizi anayeshughulikia masuala ya Syria Khaled al-Ayoubi, amesema hataki tena kuiwakilisha serikali ya Syria kwa kuwa inafanya vitendo vya ukandamizaji na vya kikatili dhidi ya watu wake yenyewe.

Kujiuzulu kwa afisa huyo kumekuja wakati vikosi vya serikali ya Syria vikiendelea na mashambulzi katika maeneo yanayoshikiliwa na wasi katika mji wa Aleppo, kwa kutumia helkopta na makombora.

Serikali inasema imeidhibiti wilaya ya Salaheddin, lakini waasi wanapinga hilo.

Ufaransa imetoa wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa dharura wa mawaziri. Rais Hollande na serikali yake wanachukua zamu ya kuwa Rais wa Baraza hilo Jumatano wiki hii na anataka wakutane mwishoni mwa wiki.