Kambi ya jeshi yavamiwa Ivory Coast

Majambazi waliokuwa wamejihami wameshambulia kambi ya kijeshi mjini Abidjan, mji mkuu wa Ivory Coast.

Wenyeji walielezea kusikia milio ya risasi usiku kucha. Idadi kubwa ya wanajeshi wakiwemo walinzi wa amani wa umoja wamataifa, wamepelekwa katika eneo hilo ingawa sasa maafisa wakuu wanasema kuwa hali imeweza kudhibitiwa.

Mji huo ulishuhudia mapambana makali, mwaka jana wakati mvutano wa kisiasa ulipotokea baada ya matokeo ya uchaguzi ambayo yalizua utata mkubwa.

Mnamo siku ya Jumapili, wapiganaji waliokuwa wamejihami walishambulia kambi ya jeshi na kuwaua wanajeshi watano katika kituo cha polisi na kambi ndogo ya kijeshi mjini Abidjan.

Wapiganaji hao walivalia sare za kijeshi na kutumia silaha nzito nzito japo hawakuweza kutambuliwa.

Sababu ya shambulio hilo pia haijajulikana.

Shambulio hilo lilitokea katika wilaya ya Yopougon ambayo inaaminiwa kuwa mojawapo ya wilaya zilizoshambuliwa zaidi na waasi wakati wa machafuko na hatimaye ushindani wa uongozi wa Abidjan kufuatia matokeo yaliyozua utata wa uchaguzi wa urais mwaka jana.