Masingasinga washambuliwa Marekani

Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, amesema ameshtushwa na kusikitishwa na shambulio lililofanywa katika hekalu la Masingasinga katika jimbo la Wisconsin nchini Marekani, ambapo watu sita wameuawa.

Mtu mwenye silaha aliwafyatulia risasi waumini ambao walikusanyika kwa ibada ya asubuhi katika mji wa Oak Creek.

Baadaye mtu huyo aliuawa na maafisa wa polisi kwa kupigwa risasi. Bado haijafahamika lengo la shambulio hilo katika hekalu la masingasinga.

Polisi wanasema wanalichukulia shambulio hilo kama vitendo vya ugaidi wa ndani.

Shambulio hilo ni jipya katika mfululizo wa mashambulio dhidi ya masingasinga wa Marekani ambao kwa makosa wanatambulishwa kama Waislamu.