Hali ya hatari yatangazwa Kogi Ngeria

Amri ya kutotembea usiku imetangazwa katika baadhi ya maeneo ya jimbo la Kogi katikati mwa Nigeria baada ya watu wenye silaha kuwaua waumini 19 katika kanisa.

Watu hao walivamia kanisa karibu na jiji la Okene jimbo la Kogi na kuwafyatulia risasi waumini wakati wa ibada siku ya Jumatatu.

Gavana wa Kogi Idris Wada amesema wauaji hao aliowaita wa kishetani watakamatwa.

Haijafahamika ni nani aliyehusika na mashambulizi hayo, lakini kundi la kiislamu lenye msimamo mkali la Boko Haram limekuwa likifanya mashambulizi kadhaa katika makanisa na maeneo mengine nchini Nigeria.

Mwandishi wa BBC Chris Ewokor aliyetembelea eneo lililoshambuliwa anasema, eneo hilo liko tete na kuna uwepo mkubwa wa vikosi vya usalama.

Ushambuliaji huo umewastua wakristo na waislamu wa eneo hilo waliloishi hapo kwa amani, anasema.

Washambuliaji walifanya mashambulizi kwa kutumia bunduki aina ya Kalashnikov kwa waumini katika kanisa la Deeper Life Bible Church katika mji wa Otite karibu na Okene.

Mchungaji wa kanisa hilo ni miongoni mwa waliouawa na wengine wengi walijeruhiwa.

Bwana Wada ametangaza amri hiyo ya hatari kwa eneo la Okene, Otite na jimbo kuu la Lokoja.

Mwandishi wetu anasema shambulio hilo limetokea katika eneo la kusini zaidi kuliko maeneo ambayo hushambuliwa zaidi na Boko Haram.

Watu wengi watakuwa na hofu kuona shambulio hilo limetokea eneo la Okene, sehemu ambayo inakutanisha eneo kuu la waislamu la kaskazini na sehemu kubwa ya wakristo eneo la kusini.

Mwezi April vikosi vya usalama vya Nigeria vilivamia kiwanda kinachosadikika cha kutengeneza mabomu eneo la Okene, na kuwaua wapiganaji wasiopungua tisa wanaosadikika kuwa wa Boko Haram.

Mwezi February kundi la Boko Haram lilisema lilishambulia gereza eneo la Kogi kwa kutumia mabomu na silaha nzito ili kuwatorosha wafungwa 119.

Lakini mashambulizi ya Boko Haram yamekuwa yakifanywa zaidi maeneo ya kaskazini. Kundi hilo linataka kuweka mfumo wa utawala wa sharia nchi nzima.