Bangi inaathiri akili kwa vijana

Imebadilishwa: 28 Agosti, 2012 - Saa 10:28 GMT

Utafiti uliodumu muda mrefu umethibitisha kuwa vijana wanaovuta bangi wanadhuru akili zao, na huenda wakapoteza ufahamu na uwezo wa kukumbuka.

Vijana walioanza kutumia bangi hiyo wakiwa na chini ya miaka ishirini walionyesha matokeo mabaya zaidi katika mitihani na kuonyesha upungufu mkubwa katika akili zao.

Utafiti huu umefanyiwa takriban watu 1,000 nchini New Zealand.

Kikundi kimoja cha kimataifa, kilichofanya utafiti huo, kiligundua kuwa vijana walioanza kutumia bangi wakiwa chini ya umri wa miaka 18 wakati akili zao zikiwa bado zinakomaa, walipoteza uwezo wao wa kufahamu mambo haraka.

Mtaalamu wa maswala hayo nchini Uingereza, alisema kuwa huenda utafiti huo, ukafafanua kwa nini watu wanoatumia bangi hawana uelewa mzuri wa mambo.

Kwa zaidi ya miaka 20 , watafiti wameweza kuwafuatilia watu wanaotumia bangi kutoka eneo la
Dunedin nchini New Zealand.

Waliwachunguza walipokuwa watoto kabla ya hata kuanza kutumia bangi na kisha kuwachunguza mara kwa mara hadi walipofika miaka 38.

Kikundi hicho hata hivyo kilizingatia mambo kama utumiaji wa pombe na sigara pamoja na madawa mengine ya kulevya pamoja na maisha yao wakiwa wanafunzi.

Waligundua kuwa wale waliokuwa wanatumia bangi kwa muda mrefu, angalau mara nne kwa wiki kila mwaka na katika umri wao wa ujana, waliathrika kutokana na kupungukiwa akili.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.