Hali yazorota nchini Syria

Imebadilishwa: 25 Septemba, 2012 - Saa 08:24 GMT

Mjumbe wa kimataifa katika mzozo wa Syria, Lakhdar Brahimi, ameielezea hali kuwa mbaya zaidi.

Ameliambia baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuwa wafungwa walikuwa wanateswa kila wakati na watu sasa wanaogopa kwenda katika hospitali za umma.

Uhaba wa chakula unatarajiwa kukithiri na turathi za nchi zinaharibiwa.

Ujerumani, ambayo inashikilia urais katika baraza hilo, imesisitiza kuwa lazima kuwe na suluhu ya kisiasa kwa mzozo wa Syria, licha ya kuwepo na kutoelewana katika umoja wa mataifa.

Naibu wazri wa mambo ya nje wa Syria, Faisal Mekdad, ameiambia BBC kuwa Syria italalamikia baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuwa Uturuki na nchi zingine katika ghuba zinachochea mapigano kwa kupeleka magaidi Syria.

Brahimi amesema hali nchini Syria ni mbaya mno na inazidi kuwa mbaya.

Lengo lake la kupatikana suluhu ya kisiasa linaonekana kutowezekana kutokana na azma ya vyama viwili kupendelea kupigana zaidi kuliko kufanya mazungumzo na kugawanyika kwa ukubwa kwa baraza la usalama.

Ameliambia baraza hilo kwamba uungwaji mkono wa pamoja wa kimataifa ni muhimu, ambapo bila ya hilo lengo lake litakuwa halina maana.

Alikiri kwamba hajapata mpango kamili lakini ana fikra kadhaa. Ameendelea kutoa tumaini kwa kusema anatarajia kupata upenyo katika siku za hivi karibuni.

Mwanadiplomasia mmoja ameeleza kuwa Brahimi aliliambia baraza hilo kuwa utawala nchini Syria uliwatazama wanamgambo kuwa sehemu ya mpango ulioungwa mkono na nchi za nje.

Upinzani umelaumu vurugu zinazoendelea nchini kutokana na miongo minne ya ugaidi wa kitaifa.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.