Hussein Mwinyi

 1. Wazanzibari sasa kupeleka malalamiko kwa Rais ki-elektroniki

  Mwinyi kipindi ya uchaguzi
  Image caption: Rais Mwinyi anasema mfumo huo ni moja ya utekelezaji wa ahadi zake kipindi cha kampeni

  Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imezindua mfumo wa kielekronik ambao utawezesha kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kueleza changamoto wanazopitia wanapokwenda kuhudumiwa katika taasisi za serikali.

  Mfumo huo uliopewa jina la “Sema na Rais Mwinyi (SNR)” unawezesha wananchi kupiga simu au kutuma ujumbe kwa njia ya tovuti.

  Aidha mlalamikaji anaweza Kuambatanisha hati, sauti na hata picha kama ushahidi wakati wa kuwasilisha malalamiko kisha mlalamikaji atapokea namba ya siri ili kufuatilia kujua lalamiko lililotolewa limefika wapi kupata ufafanuzi na afisa anayeshugulikia.

  Rais Mwinyi anasema mfumo huo ni moja ya utekelezaji wa ahadi zake kipindi cha kampeni “Baada ya kuwasikiliza Wazanzibari nilitoa ahadi ya kuwa karibu yenu kwa kusikiliza na kutatua changamoto zenu, Ahadi yangu leo imepata ufumbuzi wa kudumu baada ya kuwatengenezea wananchi mfumo wa ki-elektoniki wa malalamiko ambao nimeuzindua rasmi” amesema Rais Mwinyi.

  Pia unaweza kusoma:

  Baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanaona Rais Mwinyi ameanza vizuri katika kupambana na kero za wananchi ambazo zimedumu kwa kipindi kirefu huku wakitaka mfumo huo uwe endelevu.

  “Mfumo huu utakuwa msaada sana maana Rais hawezi kwenda kusikiliza kila mtu lakini sasa anaweza kupata malalamiko yao na hao wananchi wanaweza kutoa madukuduku yao kwa uhuru'',anasema Issa Jumaa -Mchambuzi wa siasa.

  ''Lakini kupokea kero ni jambo moja na kero kushugulikiwa ni jambo lingine''. Issa Jumaa-Mchambuzi wa siasa'', aliongeza kusema .

  Kipindi cha kampeni za uchaguzi Rais Mwinyi, alitangaza baadhi ya vipaumbele vyake ikiwa ni pamoja na kupambana na rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma kuboresha uwajibikaji kwa kupambana na uzembe wa watumishi wa serikali, ambapo ameahidi kushughulikia tatizo hilo kwa mtindo wa Rais Magufuli.