Zimbabwe

 1. Mtu aliyejifanya Makamu wa Rais wa Zimbabwe akamatwa baada ya kutibiwa

  Mtu huyo anayetuhumiwa kuwa mlaghai kwa kujifanya kuwa Makamu wa Rais Constantino Chiwenga, aliyeonekana hapa kwenye sherehe yake ya kuapishwa mnamo 2018
  Image caption: Mtu huyo anayetuhumiwa kuwa mlaghai kwa kujifanya kuwa Makamu wa Rais Constantino Chiwenga, aliyeonekana hapa kwenye sherehe yake ya kuapishwa mnamo 2018

  Mwanamume mmoja raia wa Zimbabwe ameshtakiwa kwa ulaghai baada ya kujifanya Makamuwa rais wa nchi hiyo na kupata huduma ya matibabu bila malipo.

  Mahakama katika mji mkuu wa Harare, alifahamishwa kuwa Marlon Katiyo, 35, alitembelea hospitali mbili mara kadhaa mwezi uliopita kupata matibabu ya maumivu ya kichwa akisema kwamba alikuwa, Makamu wa Rais Constantino Chiwenga.

  Bwana Katiyo, amabye hajatoa tamko lolote kuhusiana mashtaka hayo alipewa matibabu ya bure.

  Ombi la dhamana alilowasilisha linatarajiwa kusikizwa siku ya Ijumaa.

 2. Zimbabwe: Mwanaume akamatwa baada ya msichana kufariki akijifungua kanisani

  UN imeshutumu tabia ya ndoa za utotoni
  Image caption: UN imeshutumu tabia ya ndoa za utotoni

  Polisi nchini Zimbabwe imemkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 26 baada ya msichana kufariki dunia wakati anajifungua kanisani, kesi ambayo imesababisha hasira miongoni mwa raia na wanaharakati wanaotetea haki za binadamu.

  Anna Machaya, 15, anaripotiwa kufariki na kuzikwa mwezi uliopita katika kaburi lililo kanisani eneo la mashariki mwa Marange.

  Polisi pia wamewakamata wazazi wake.

  Kesi hiyo imeweka wazi unyanyasaji wa watoto kwani inaripotiwa alilazimishwa kuacha shule ili aolewe.

  Wazazi wa Anna wanashutumiwa kwa kusema uongo juu ya umri wake na pia waliahidi binti yao wa miaka tisa kumuozesha kwa mtu huyo huyo, Hatirarami Momberume.

  Mwanaume huyo anakabiliwa na mashtaka ya ubakaji wa watoto.

  Washtakiwa hao watatu bado hawajatoa maoni yao kuhusiana na tukio hilo.

  Kifo cha Anna kilichotokea Julai 15, siku chache baada ya siku yake ya kuzaliwa, kimeweka angalizo juu ya tabia ya ndoa za utotoni katika Kanisa maarufu la Apostolic Church nchini Zimbabwe, ambalo mara nyingi hukataa utumiaji wa dawa na matibabu hospitalini.

 3. Binti aliyefia kanisani wakati akijifungua, aibua ghadhabu kali Zimbabwe

  Umoja wa Mtaifa umelaani vikali ndoa za utotoni
  Image caption: Umoja wa Mtaifa umelaani vikali ndoa za utotoni

  Polisi nchini Zimbabwe wanachunguza kifo cha msichana mwenye umri wa miaka 14-kilichotokea wakati anajifungua, kesi hiyo imeibua hisia mbalimbali miongoni mwa wananchi na wanaharakati wa haki za binadamu. Memory Machaya ameripotiwa kufariki mwezi uliopita katika madhabau mashariki mwa mji wa Marange.

  Kesi hiyo imeelezewa kuwa ni unyanyasaji wa watoto, binti huyo aliripotiwa kulazimishwa kuacha shule ili aolewe. Umoja wa Mataifa umetaka serikali kuidhinisha kuwa mimba za utotoni ni uhalifu na kusitisha utamaduni huo. Shirika hilo limesema wasiwasi wake mkubwa na kulaani vikali ripoti kuhusu kifo cha binti huyo. Shirika hilo limesema "linatoa maelezo juu ya wasiwasi wake mkubwa" na "limelaani vikali" ripoti zinazoelezea jinsi kifo kilivyojitokeza.

  "Hali iliyopo sasa ya kutotatua kesi za unyanyasaji kwa wanawake na wasichana nchini Zimbabwe, zikiwemo kesi za ndoa za utotoni, haiwezekani kuendelea kupuuziwa," taarifa ya UN ilieleza siku ya Jumamosi. Kifo cha binti huyo kilichotokea Julai 15, kimetoa angalizo juu ya mimba za utotoni katika kanisa la Zimbabwe Apostolic ,ambalo limekuwa linakataa dawa na tiba za hospitalini.

  Familia yake ilisema mtoto alipona na alijifungua salama, vyombo vya habari vya ndani vimeripoti. Mazingira ambayo yalipelekea kifo chake kuchunguzwa na polisi na tume ya jinsia nchini humo.

  Baadhi ya watu waliandika maombi yao mtandaoni kwa kutaka haki itendeke juu ya kifo cha binti huyo Memory Machaya" mpaka sasa saini za watu zaidi ya 57,000 zinataka haki ipatikane. Mwanaharakati wa Zimbabwe wa kutetea haki za wanawake bi. Everjoice Win alisema ni wakati muafaka kwa watu kuweka msukumo kwa walio madarakani kuweka sheria mpya. Wanawake na wasichana hawaonekani kama binadamu waliokamilika wenye haki ... na kuwa na mamlaka ya miili yao" aliandika kwenye Twitter. Kisheria, wasichana wa Zimbabwe wanaruhusiwa kuolewa wakiwa na miaka 18, wakati miaka 16 kuwa na idhini ya kujamiiana.

  Lakini baadhi ya familia wanaamini kuwa ndoa za utotoni zina manufaa ya kifedha.

  Mabinti wengi wanaoolewa wakiwa wadogo wana matumaini kuwa ndoa itawapatia fursa ya kwenda shule. Hata hivyo , mabinti hao huishia kupata mimba mara tu baada ya kuolewa na hivyo kubaki kuwa mama wa nyumbani.

 4. Chifu aamuru mwili wa Mugabe kufukuliwa na kuzikwa upya

  Mugabe

  Kiongozi wa kitamaduni nchini Zimbabwe ameaamuru kwamba mabaki ya rais wa zamani wa nchi hiyo Robert Mugabe yafukuliwe na kuzikwa katika makaburi ya kitaifa.

  Mugabe alifariki mwaka 2019 na alizikwa nyumbani kwake Kutama kulingana na ombi lake na wala sio katika makaburi ya mashujaa wa kitaifa katika mji mkuu, Harare, kama alivyotarajia mrithi wake Rais Emmerson Mnangagwa na wengine.

  Familia yake imesema Mugabe alikuwa ameelezea hofu yake kwamba mahasimu wake wa kisiasa waliomuondoa madarakani mwaka 2017 huenda wakatumia mabaki yake kufanya kafara ikiwa atazikwa katika makaburi ya kitaifa.

  Siku ya Jumatatu, chifu wa kitamaduni katika wilaya ya Zvimba, magharibi mwa mji mkuu wa Harare, alisema kwamba amepokea malalamishi kutoka kwa jamaa wa ukoo wa Mugabe kuhusu mahali alipozikwa.

  Aliamua kuwa Grace Mugabe alikuwa na makosa kwa kukiuka muongozo wa kimila kwa kumzika mume wake nyumbani kwake.

  Bi Mugabe hakufika mbele ya kikao hicho, lakini chifu alimpiga faini ya kulipa ng’ombe watano na mbuzi mmoja.

  "Yeye [chifu] hana mamlaka dhidi ya Kutama. Na hata kama chifu alifanya uamuzi sahihi tungelikata rufaa mahakamani," Leo Mugabe, msemaji wa familia, aliliambia shirika la habari la Reuters.

 5. Mke wa Mugabe ashtakiwa kwa mazishi ‘yasiyofaa’ ya rais Mugabe

  mugabe

  Mke wa rais wa zamani wa Zimbabwe Grace Mugabe, ameagizwa kufika mbele ya mahakama ya kitamaduni kwa tuhuma za kufanya mazishi “yasiyofaa” ya hayati Rais Robert Mugabe.

  Grace Mugabe anatuhumiwa kwa kuenda kinyume na utamaduni wa jamii yao kwa kumzika mume wake katika boma la familia badala ya kumzika “sehemu iliyochaguliwa na jamaa zake na mama yake".

  Katika waraka kutoka kwa Chifu Zvimba, ambaye ni mkuu wa kitamaduni wa nyumbani kwa kina Mugabe, Mke wake Grace anatakiwa kuufukua mwili wa hayati Rais Mugabe ili uzikwe tena “kulingana na utamaduni wa watu wa Zvimba".

  Pia ameagizwa kulipa faini ya ng’ombe na mbuzi kwa kukiuka utamaduni.

  Mugabe alifariki mwaka 2019 katika hospitali moja nchini Singapore akiwa na umri wa miaka 95.

  Familia yake iliamua afanyiwe mazishi ya faragha kijijini kwao Kutama wilaya ya Zvimba- karibu kilomita 90 sawa na (maili 55) magharibi mwa mji mkuu wa Harare – baada ya mvutano wa wiki kadhaa na serikali.

  Patrick Zhuwao, mpwa wa marehemu rais, siku ya Alhamisi aliiambia televisheni ya Shirika la utangazaji la Afrika Kusini kwamba Mugabe alizikwa kulingana na ombi lake, uamuzi ambao unastahili kuheshimiwa.

  Amesema hakuna mzozo ndani ya familia akiongeza kwamba suala hilo lipo nje ya mamlaka ya chifu.

 6. Rais wa zimbabwe awasili kutoa heshima ya mwisho kwa hayati rais Magufuli

  X

  Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe tayari amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho kwa hayati Magufuli hapo kesho jijini Dodoma.

  Mnangagwa ni miongoni mwa marais 10 wanaotarajiwa kuhudhuria shughuli za kuaga mwili wa hayati John Pombe Magufuli katika Uwanja wa Jamhuri, uliopo mji mkuu wa Tanzania Dodoma.

  Marais wengine ni kutoka Kenya, Zambia, Morocco, Namibia, Malawi ,Botswana , Afrika Kusini na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

  Kwa upande wa waliotuma wawakilishi ni Waziri Mkuu wa Rwanda, waziri wa mambo ya nje wa Angola, Makamu wa Rais wa Burundi pamoja na wawakili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Muungano wa Mataifa ya Kusini mwa Afrika SADC, Mabalozi na kutoka Umoja wa Mataifa.

 7. Mke wa Rais wa Zimbambwe atoa wito wa maombi na kufunga

  Auxillia Mnangagwa alikuwa mama wa taifa wa Zimbabwe November 2017

  Mama wa taifa nchini Zimbabwe ametoa wito kwa wanawake nchini humo kuungana naye katika ibada ya kufunga na maombi kwa siku tatu kwasababu ya janga la virusi vya corona.

  Auxillia Mnangagwa amesema kuwa atafunga na kuomba kuanzia Alhamisi hadi Jumamosi nchini Zimbabwe akiomba "kuepukana na janga hilo".

  Mama wa taifa hilo amesihi wanawake kuhakikisha familia zinazingatia sheria za kuzuia ugonjwa wa corona.

  "Tunahitajika kuwa na mpango madhubuti majumbani kuhakikisha usafi wa mara kwa mara ili kila mmoja nyumbani anajua umuhimu wa kuvaa barakoa sahihi, cha msingi zaidi kuwepo na kuzingatia kila mmoja anakuwa salama na familia kusalia nyumbani," taarifa hiyo inasema.

  Zimbabwe imethibitisha kufariki dunia kwa watu 879 kutokana na virusi vya corona, ikiwemo maafisa wa serikali na wiki hii Waziri wa mambo ya nje Sibusiso Moyo amefariki dunia.

  Nchi hiyo imethibitisha maambukizi 29,408 ya virusi vya corona huku watu 19,253 wakipona.

 8. Video content

  Video caption: Zimbabwe: Jamii inayopata maji kutoka makaburini

  Kuna hofu maji hayo huenda yamechanganyika na uchafu kutoka kwa miili ya watu waliozikwa hapo