Senegal

 1. Wanamieleka Senegal 'wakanusha madai ya kushiriki maandamano'

  Wanamieleka wa Senegal wamekanusha madai ya kwamba wamejihusisha na maandamano

  Wanamieleka wa Senegal wamekanusha madai ya kwamba wamejihusisha na maandamano ya hivi karibuni yaliyokumba nchi hiyo ya Afrika Magharibi, kulingana na taarifa kutoka Shirika la Habari la AFP.

  Wanamieleka, ambao wanaheshimika sana nchini Senegal, wamekasirishwa na taarifa kwamba walihusika na maandamano yaliyosababisha vifo vya watu wanane.

  Katika mitandao ya kijamii, baadhi ya watu wameshutumu serikali kwa kukodi wanamieleka kusababisha fujo.

  Shirika la Habari la AFP limemnukuu Waziri wa Haki Malick Sall aliyesema kuwa wanamieleka walihusika kwenye maandamano wakati nchi ilikuwa imeweka kanuni za kukabiliana na virusi vya corona.

  "Vijana, wengi wao walikuwa ni wanamieleka...hili liliwafanya sio tu kuchangamka lakini pia kupata ajira," Bwana Sall alisema hivyo katika mahojiano.

  Khadim Gadiaga, mkuu wa wanamieleka wanaoheshimiwa katika mji wa Dakar wamekanusha madai hayo. "Hakuna hata mwanamieleka mmoja aliyeshiriki maandamano," Shirika la AFP limemnukuu wakisema hivyo.

  Maandamano nchini Senegal katika wiki za hivi karibuni yamechochewa na kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani Ousmane Sonko, ambaye anashutumiwa kwa madai ya ubakaji – ambayo mwenyewe anasema yamechochewa kisiasa.

 2. Televisheni za Senegal zafungwa kwasababu ya kuangazia maandamano

  Wafuasi wa kiongozi wa upinzani wa Senegal walikabiliana na polisi
  Image caption: Wafuasi wa kiongozi wa upinzani wa Senegal walikabiliana na polisi

  Mamlaka nchini Senegal zimesitisha matangazo ya vituo viwili vya televisheni za kibinafsi baada ya kuzilaumu kwa kuangazia zaidi maandamano yaliyosababishwa na kukamatwa kwa kiongozi wa upinzani, Ousmane Sonko.

  Vituo viwili vilivyoathirika na uamuzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Matangazo nchini humo ni Sen TV na Walf TV.

  Vituo hivyo vimeshutumiwa kwa upeperushaji wa picha zinazoonesha maandamano baada ya Bwana Sonko kukamatwa, Shirika la habari la AFP limeripoti.

  Siku ya Alhamisi, polisi walikabiliana na wafuasi wa Bw. Sonko mjini Bignona kusini mwa eneo la Casamance.

  Serikali imethibitisha kuwa mtu mmoja aliuawa siku ya katika ghasia za Alhamisi zilizotokana na kukamatwa na Bw. Sonko mjini Dakar mapema siku hiyo.

  Bw. Sonko amelaumiwa kwa kumbaka mwanamke mmoja katika saluni ambako alikwenda kusingwa.

 3. Papa Bouba Diop afariki dunia

  Papa Bouba Diop

  Aliyekuwa kiungo wa kati wa Senegal, Fulhama na Portsmouth Papa Bouba Diop amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 42.

  Diop alijitokeza mara 129 katika Ligi ya Premier na pia aliwahi kuchezea Uingereza katika timu za West Ham United na Birmingham City.

  Alichezea Senegal mwaka 2002 katika Kombe la Dunia na kufunga bao lililowafanya kuibuka na ushindi katika mechi ya ufunguzi baada ya Senegal kuichabanga Ufaransa bao moja kwa nunge.

  "Ukishakuwa shujaa wa Kombe la Dunia mara moja, siku zote unakuwa shujaa wa Kombe la Dunia," Fifa imeandika ujumbe huo katika mtandao wa kijamii.

  Ujumbe uliotumwa katika mtandao wa Twitter na klabu ya Fulham umesema kuwa klabu hiyo "umeshutushwa" na taarifa za kifo chake na pia wametumia jina la utani la Diop: "Lala salama, Wardrobe."

  Senegal ilifika robo fainali katika kombe la dunia la mwaka 2002 huku Diop akifunga mara mbili zaidi katika mechi ya makundi iliyotoka sare ya 3-3 na Uruguay.

  Pia amewahi kushiriki katika mashindano ya Kombe la Afrika ikiwemo wakati Senegal ipokuwa ya pili mwaka 2002. Diop alistaafu soka mwaka 2013.

 4. Baba akamatwa baada ya mtoto wake kufa na kutupwa baharini

  Senegal imeshuhudia ongezeko la wahamiaji wakijaribu kwenda Ulaya

  Polisi nchini Senegal wamemkamata baba wa mtoto wa kiume wa miaka 15 aliyekufa maji baharini mwezi Oktoba wakati akijaribu kwenda Ulaya.

  Inadhaniwa kuwa baba alimlipa fedha msafirishaji kiasi cha pauni 340 kumpeleka mtoto wake Uhispania.

  Mtoto huyo kwa jina jingine Doudou,kisha angechukuliwa kwenda Italia katika kituo cha mafunzo ya mpira wa miguu.

  Aliugua, na kupoteza maisha akiwa njiano na mwili wake ulitupwa baharni.

  Kifo chake kilisababisha mshtuko nchini Senegal, ambayo hivi karibuni imeshuhudia ongezeko la wahamiaji wakijaribu kuvuka bahari kufikia Ulaya.

  Polisi wa Senegal walisema wamewakamata wahamiaji zaidi 1,500 katika siku za hivi karibuni.

 5. Akon kusonga mbele na ujenzi wa 'Akon City' Senegal

  Akon

  Msanii Akon wa muziki wa R&B nchini Marekani na ambaye amekuwa akizungumzia kujenga mji mpya nchini Senegal tangu 2018 amesema shughuli ya ujenzi itaanza mwaka ujao.

  Akon hakuwatambulisha wawekezaji katika mradi huo lakini amefichua kwamba ufadhili wa thuluthi tatu ya dola bilioni sita umepatikana.

  Mchoraji ramani wa mji huo mpya, Hussein Bakri, amesema idadi ya watu katika mji huo inakadiriwa kufika 300,000.

  Akon, ambaye jina lake halisi ni Alioune Badara Thiam, aliwashirikisha moja kwa moja Wamarekani weusi katika mauzo ya mradi huo.

  Alisema kuwa ametangamana na "Waafrika wenye asili ya Marekani ambao hawaelewi utamaduni wao, Kwa hivyo nilitaka kujenga mji ama kubuni mradi kama huu ambao utawapa motisha ya kuwa na makazi katika nchi yao," Shirika la habari la AFP lilimnukuu msanii huyo aliyezaliwa Marekani kutokana na wazazi raia wa Senegal, akisema.

  "Unapoamua kuishi Marekani,Ulaya ama mahali kwengine ughaibuni na ungelipendelea kuzuru Afrika, tunataka Senegal iwe kituo chako cha kwanza," alisema.