Mzozo Zimbabwe

 1. Chifu aamuru mwili wa Mugabe kufukuliwa na kuzikwa upya

  Mugabe

  Kiongozi wa kitamaduni nchini Zimbabwe ameaamuru kwamba mabaki ya rais wa zamani wa nchi hiyo Robert Mugabe yafukuliwe na kuzikwa katika makaburi ya kitaifa.

  Mugabe alifariki mwaka 2019 na alizikwa nyumbani kwake Kutama kulingana na ombi lake na wala sio katika makaburi ya mashujaa wa kitaifa katika mji mkuu, Harare, kama alivyotarajia mrithi wake Rais Emmerson Mnangagwa na wengine.

  Familia yake imesema Mugabe alikuwa ameelezea hofu yake kwamba mahasimu wake wa kisiasa waliomuondoa madarakani mwaka 2017 huenda wakatumia mabaki yake kufanya kafara ikiwa atazikwa katika makaburi ya kitaifa.

  Siku ya Jumatatu, chifu wa kitamaduni katika wilaya ya Zvimba, magharibi mwa mji mkuu wa Harare, alisema kwamba amepokea malalamishi kutoka kwa jamaa wa ukoo wa Mugabe kuhusu mahali alipozikwa.

  Aliamua kuwa Grace Mugabe alikuwa na makosa kwa kukiuka muongozo wa kimila kwa kumzika mume wake nyumbani kwake.

  Bi Mugabe hakufika mbele ya kikao hicho, lakini chifu alimpiga faini ya kulipa ng’ombe watano na mbuzi mmoja.

  "Yeye [chifu] hana mamlaka dhidi ya Kutama. Na hata kama chifu alifanya uamuzi sahihi tungelikata rufaa mahakamani," Leo Mugabe, msemaji wa familia, aliliambia shirika la habari la Reuters.

 2. Video content

  Video caption: Zimbabwe: Jamii inayopata maji kutoka makaburini

  Kuna hofu maji hayo huenda yamechanganyika na uchafu kutoka kwa miili ya watu waliozikwa hapo

 3. Waziri wa Zimbabwe adai upinzani una njama ya kuingiza silaha nchini

  Emmerson Mnangagwa
  Image caption: Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa

  Waziri wa usalama wa kitaifa wa Zimbabwe, Owen Ncube, anadai kuwa upinzani unafanya kazi na nchi za magharibi kuingiza silaha kimagendo nchini humo kwa lengo la kumuondoa madarakani Emmerson Mnangagwa.

  Maafisa kutoka chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change hata hivyo wamepuuza madai hayo wakisema kuwa hayana msingi wowote.

  Bila kutoa ushahidi, Bw. Ncube amesema nchi za Magharibi ambazo hakuzitaja zimekuja na mkakati wa kuvuruga utawala wa Zimbabwe ili wathibitishe haja mataifa ya kigeni kuingilia kati kutatua mzozo.

  Makundi ya kutetea haki yanasema serikali ya Rais Mnangagwa imekuwa ikikosolewa vikali hasa wakati huu ambapo mzozo wa kiuchumi wa nchi hiyo unaendelea kufukuta.

  Wamelaani hatua ya hivi karibuni ya kufungwa kwa wanasiasa na wanaharakati kwa kile walichodai kuwa mashitaka ya uongo.

 4. Zimbabwe kuwafidia wazungu waliopokonywa mashamba yao

  Wakulima wazungu 3,500 walifurushwa kutoka kwa mashamba yao karibu miaka 20 iliyopita
  Image caption: Wakulima wazungu 3,500 walifurushwa kutoka kwa mashamba yao karibu miaka 20 iliyopita

  Serikali ya Zimbabwe imesema kwamba wakulima wazungu ambao walipokonywa ardhi zao kati ya mwaka 2000 na 2001 wanaweza kutoa maombi ya kurudishiwa ardhi hizo chini ya mpango mpya wa mageuzi ya sera ya ardhi.

  Ikiwa ardhi haitaweza kurudishwa, wakulima hao watapewa ardhi sehemu nyingine, kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na Mawaziri wa Fedha Mthuli Ncube na wa Ardhi Anxious Masuka.

  Mawaziri hao wamesema watafutilia mbali barua zilizowapa idhini wakulima weusi kuchukua ardhi hizo.

  Walisema wakilima wazungu ambao ardhi zao zilichukuliwa na serikali na ambazo hazijatolewa wanaweza kutoa maombi ya kuzikodisha kwa miaka 99.

  Wakulima wazungu 3,500 walifurushwa kutoka kwa mashamba yao wakati wa marekebisho tata ya sera ya ardhi.

  Serikali ya Zimbabwe mwezi Mei ilikubali kuwafidia dola bilioni 3.5 wakulima wazungu ambao ardhi zao zilichukuliwa enzi za utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo marehemu Robert Mugabe.