Afrika Kusini

 1. Afrika Kusini yapiga marufuku uuzaji wa pombe

  Rais Ramaphosa anasema unywaji pombe unachangia tabia ya uzembe
  Image caption: Rais Ramaphosa anasema unywaji pombe unachangia uzembe

  Serikali ya Afrika Kusini imepiga marufuki uuzaji wa pombe wa kwenda nayo nyumbani wikendi hii ya Pasaka, kuzuia ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona .

  Rais Cyril Ramaphosa amesema pombe inachangia tabia ya kutojali na uzembe.

  Mabaa na migahawa hata hivyo huenda zikaruhusiwa kuuza vinywaji

  Mikusanyiko ya kidini pia imedhibitiwa kwa hadi asilimia 50 ikiwa inafanyika ndani ya jengo.

  Maambukizi ya corona yamepungua Afrika Kusini baada ya wimbi la pili la maambukizi kupanda mwezi Januari.

  Marufuku dhidi ya uuzaji pombe imewekwa mara kadhaa tangu janga la corona lililipoanza.

 2. Kifo cha Rais Magufuli: Afrika Kusini yaungana na Tanzania katika maombolezo

  south

  Raisi wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ameeleza masikitiko yake kufuatia kifo cha Rais wa Tanzania, John Magufuli.

  Katika taarifa yake, raisi Ramaphosa amesema amezungumza na Makamo wa Raisi wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akimweleza huzuni yake na kwa niaba ya raia wa Afrika Kusini.

  ‘’Afrika Kusini inaungana na serikali na watu wa Tanzania katika kipindi hiki kigumu’’alisema.

  View more on twitter
 3. Mwalimu mkuu Afrika Kusini 'amemlazimisha mtoto kutafuta simu kwenye shimo la choo'

  Serikali imeahidi kuondokana na vyoo vya mashimo katika shule za serikali (Picha iliyokuwa imehifadhiwa)

  Mwalimu mkuu wa shule moja nchini Afrika Kusini amesimamishwa kazi kwa madai ya kumlazimisha mwanafunzi kijana wa miaka 11 kutafuta simu kwenye shimo la choo.

  Inadaiwa kwamba mwalimu huyo alimshukisha mwanafunzi huyo kwenye shimo la choo kwa kutumia kamba akimuahidi randi 200 sawa na dola 14 za Marekani.

  Bibi ya kijana huyo amesema mjukuu wake anaogopa kwenda shuleni kwasababu wanafunzi wengine wanamdhihaki.

  Bodi ya elimu ya eneo imezungumza na gazeti la TimesLive na kusema tukio hilo ni "aibu".

  Vyoo vya mashimo nchini Afrika Kuusini ambapo mwaka jana vilikadiriwa kuwa sudusi au moja ya sita ya shule zote bado vinatumika licha ya kwamba ni hatari.

  Afisa wa juu wa elimu eneo la Mashariki la Cape, Fundile Gade, amewaambia wananahabari kuwa tukio hilo lilikuwa "zaidi ya aibu" na atamtembelea mwanafunzi huyo nyumbani kwao kuomba msamaha.

  Mwalimu mkuu anayedaiwa kutekeleza hayo katika shule ya Luthuthu Junior sasa hivi anachunguzwa na idara ya Cape ya Mashariki na hatua stahiki zitachukuliwa.

  Inasemekana kuwa pia alihamasisha watoto wengine kusaidia kutafuta simu hiyo ambayo inadaiwa ilianguka kwa bahati mbaya katika choo cha walimu mwanzoni mwa Machi.

  Vyombo vya habari vya eneo vimesema tukio hilo lilijulikana baada ya shirika lisilo la serikali ambalo linafanyakazi ya kuhamsisha umuhimu wa kwenda shuleni kusikia kuhusu kisa hicho.

  Petros Majola, kutoka shirika la jamii la Khula aliweka video mtandaoni ambayo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii inayoonesha kuwa utafutaji wa simu hiyo uliendelea kwa saa moja.

  Baada ya baadhi ya wanafunzi kutumia ndoo kupunguza kinyesi ndani ya shimo hilo la choo, Bwana Majola amenukuliwa akisema kwamba kijana huyo alishukishwa kwa kamba hadi "magoti yake yakawa yameingia ndani ya kinyesi".

  "Alitumia mikono yake kutafuta simu hiyo huku kinyesi kikimfikia juu ya mikono yake na kiwiko cha mkono."

  Kulingana na taarifa za News24, baada ya simu hiyo kukosekana, mwalimu mkuu alimpa mtoto huyo randi 50 kwa juhudi zake.

  Bibi yake kijana huyo amesema kuwa mjuu wake aliona aibu sana kurejea shuleni baada ya kitendo hicho.

 4. Mflame wa Wazulu Goodwill Zwelithini afariki Afrika Kusini

  Mfalme Goodwill Zwelithini (kulia) alikuwa akipokea tiba ya ugonjwa wa kisukari
  Image caption: Mfalme Goodwill Zwelithini (kulia) alikuwa akipokea tiba ya kisukari

  Mfalme Goodwill Zwelithini wa jamii ya Wazulu nchini Afrika Kusini amefariki hospitalini ambako alikuwa anapokea tiba ya kisukari.

  Mfalme huyo aliyekuwa na umri wa miaka 72, alikuwa kiongozi wa kabila kubwa zaidi Afrka Kusini na kiongozi mashuhuri wa kitamaduni.

  Alikuwa amelazwa katika hospitali ya KwaZulu-Natal wiki iliyopita kufuatilia hali ya kisukari iliyokuwa inamkabili.

  Waziri mkuu wa mfalme huyo ameishukuru Afrika Kusini kwa "kuendelea kumuombea na kutoa msaada kipindi hiicho kigumu".

  Mflame Goodwill Zwelithini aliongoza jamii ya Wazulu chini ya kifungu cha sheria ya utawala wa kitamaduni katika katiba ya Afrika Kusini tangu alipofariki baba yake mwaka 1968.

  Karibu watu milioni 10 wanaishi katika mkoa wa KwaZulu-Natal.

 5. Simba wamshambulia na kumuua afisa wa wanyamapori Afrika Kusini

  Simba

  Mtu mmoja amefariki baada ya kushambuliwa na simba wawili katika hifadhi ya wanyama nchini Afrika Kusini, mamlaka zimesema siku ya Jumatatu.

  Malibongwe Mfila, 27, ambaye alifanya kazi ya kufuatilia mienendo ya wanyama katika mbuga ya kitaifa ya wanyama ya Marakel,amekuwa akiwatafuta wanyama katika mbuga hiyo siku ya Jumamosi aliposhambuliwa na simba hao.

  Polisi wanasema alikuwa akiendesha gari kuwatafuta wanyama kama vile simba na tembo ili kutoa ushauri kwa wanaowaelekeza watalii mbugani.

  Aliamua kuacha gari na kuendelea kuwatafuta wanyama kwa miguu "mara ghafla akashambuliwa na simba wawili hadi akafariki," polisi waliongeza.

  Simba hao pia waliuawa kwa kupigwa risasi.

  Mwaka jana mtunzaji mashuhuri wa Afrika Kusini Mathewson Magharibu, alifariki baada ya kushambuliwa na simba alipokuwa akiwapeleka matembezi wageni katika hifadhi ya wanyama ya Limpopo.

 6. Tanzania, Afrika Kusini na Nigeria zawekewa marufuku ya muda ya usafiri Oman

  Air Tanzania

  Wasafiri wanaoingia Oman kutoka nchi 10 wamepigwa marufuku ya kuingia nchini humo.

  Nchi zilizopigwa marufuku ni Tanzania Afrika Kusini, Lebanon, Sudan, Brazil, Nigeria, Guinea, Ghana, Sierra Leone, na Ethiopia.

  Marufuku hiyo itaanza kutekelezwa usiku wa Alhamisi wiki hii na itadumu kwa siku 15.

  Hatua hiyo imetokana na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya udhitibi wa Corona nchini humo.

  Kamati hiyo imesema uamuzi huo ni wa kupambana na maambukizi ya Corona.

  Marufuku hiyo pia inawahusisha watu watakaopita katika nchi hizo ndani ya siku 14 kabla ya kuingia Oman.

  Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Oman, mkutano wa kamati hiyo uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa Oman Hammoud bin Faisal Al Busaid.

  Kamati hiyo imewataka wananchi wa Oman kutosafiri nje ya nchi ili kuzuia maambukizi na ikibidi kusafiri basi kuwe na sababu maalum.

  Maelezo zaidi:

  Magufuli: 'Hatujazuia matumizi ya barakoa'

 7. Mwanasisa wa upinzani wa Rwanda auawa Afrika Kusini

  Seif Bamporiki
  Image caption: Seif Bamporiki

  Mwanasiasa wa upinzani na raia wa Rwanda anayeishi mafichoni nchini Afrika Kusini ameuawa kwa kupigwa risasi.

  Ripoti zinasema Seif Bamporiki aliuawa alipokuwa akiwasilisha samani kwa mteja Jumapili mchana mjini Cape Town. Haijabainika kama kifo chake kilichochewa kisiasa.

  Waliomvamia walichukua simu zake za rununu na pochi kabla ya kutoroka eneo la tukio.

  Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na kisa hicho.

  Bunduki

  Bw. Bamporiki alikuwa mshirikishi wa chama cha Rwanda National Congress.

  Msemaji wa chama hicho, Etienne Mutabazi, ameiambia BBC kwamba mteja alikuwa amewasiliana na Bw. Bamporiki – ambaye anaendesha duka la kuuza vitanda – kuuliza kama ana kitanda cha kuuza.

  Mteja kisha aliomba kitanda hicho kupelekwa katika mji wa Nyanga na kuamua kutumia gari na Bwana Bamporiki na mwenzake kwenda eneo ambalo kitanda kilitakiwa kupelekwa.

  Maelezo ya kile kilichotokea baada ya hapo bado hayajathibitishwa, lakini Bw. Bamporiki aliuawa kwa risasi moja ambayo ilipigwa kupitia dirisha la gari.

  Mji wa Nyanga unafahamika kuwa moja ya miji hatari nchini Afrika Kusini.

  Wakati mmoja ulikuwa na idadi ya juu zaidi ya mauaji kwa mwaka.