Misaada ya Kimataifa

 1. Ethiopia yapanga kufunga kambi za wakimbizi Tigray

  Mapigano yalitokea katika eneo Tigray Novemba mwaka jana.

  Ethiopia inapanga kufunga kambi mbili za wakimbizi zilizopio kaskazini mwa jimbo la Tigray ambalo lilikumbwa na vita kati ya waliokuwa watawala (TPLF) na serikali kuu, kwa mujibu wa shirika la wakimbizi nchini humo.

  Akizungumza na wanahabari Jumanne, mkuu wa Shirika la Wakimbizi na Wanaorejea nchini Ethiopia, Tesfaye Gobezay, amesema ukaribu na mipaka ya Eritrea na hali mbaya ya kijiographia ndizo sababu zilizopeekea kufungwa kwa kambi hizo.

  Karibu wakimbizi 100,000 kutoka Eritrea walikuwa wanaishi kambini huko Tigray kabla ya kuanza kwa mapigano mapema mwezi Novemba.

  Kambi mbili - Shimbela na Hitsats – ambazo zilikuwa na zaidi ya wakimbizi 20,000 hazijaweza kufikiwa kwa ajili ya kupewa misaada siku za hivi karibuni.

  Bwana Tesfaye aliongeza kuwa wakimbizi watapelekwa katika kambi zingine au kurejeshwa wenye jamii.

  Hivi karibuni, shirika la UN lilisema kwamba karibu wakimbizi 20,000 wa Eritrea hawajulikani walipo.

  Kulingana na Bwana Tesfaye kumekuwa na majaribio ya awali ya kufunga kambi za Hitsats, lakini juhudi hizo zikashindikana kwasababu chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kilipinga mpango huo na pia janga la corona likachangia.

  “Kulikuwa na mapigano haswa katika kambi hizo” na wakimbizi “walijikuta katika njia panda”,Bwana Tesfaye alisema.

  Hata hivyo uchunguzi zaidi unahitajika kubaini taarifa za kina na ikiwa kuna waliopoteza maisha yao.

 2. MSF:'Inasikitisha kufikia uamuzi wa kusitisha msaada tunaotoa'

  MSF

  Shirika la Madaktari wasio na mipaka - MSF limelazimika kufanya maamuzi magumu ya kusitisha msaada wake wa kiafya eneo la Fizi hasa kambi ya Baraka, kusini mwa mkoa wa Kivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

  Hatua hiyo inawadia baada ya kuondoa wafanyakazi wake wengi eneo la hilo mnamo mwezi Julai kufuatia matukio kadhaa ya ghasia dhidi ya shirika hilo.

  “Inasikitisha kuona tumefikia uamuzi wa kusitisha msaada tunaotoa kiasi kikubwa,” mkuu wa shirika la MSF, Ellen van der Velden amesema. “Sio jambo rahisi lakini baada ya matukio kadhaa ya ghasia dhidi wafanyakazi wetu eneo la Fizi, utabiri wa uwezekano wa kutokea kwa matukio mabaya zaidi ya kudhuru wafanyakazi wetu ni jambo lisilokubalika.”

  Uhalifu unaozidi kuongezeka unaotekelezwa na makundi yaliyojihami mashariki mwa DRC, kumesababisha kutokea kwa ghasia dhidi ya raia ikiwemo mauaji, ghasia mbaya na unyanyasaji wa kingono na kupelekea athari kubwa kwa mamilioni ya watu ikiwemo kutoroka makazi yao.

  Hata hivyo, Shirika hilo la Madaktari wasio na mipaka - MSF limesema bado limejitolea kusaidia raia wa DRC na kuongeza kuwa katika eneo lililoathirika la Fizi hasa Baraka na Kimbi, bado litaendelea kutoa msada wake wa kiafya hadi robo ya kwanza ya 2021.