Sekta ya Mafuta na Gesi

 1. Mashambulizi ya kijeshi Msumbiji 'yanayokabiliwa na changamoto'

  Mwezi uliopita Rwanda ilituma wanajeshi wake 1,000 kwenda Msumbiji kupigana na wanamgambo
  Image caption: Mwezi uliopita Rwanda ilituma wanajeshi wake 1,000 kwenda Msumbiji kupigana na wanamgambo

  Mkuu wa jeshi la Msumbiji amesema shambulio linaloendelea katika mkoa wa kaskazini wa Cabo Delgado limekabiliwa na upinzani kidogo kwasababu wapiganaji walioko huko labda huenda walitupilia mbali silaha zao na kujifanya kama raia.

  "Ndiyo sababu tunaendelea kuwafuata na kufanya uchunguzi kwa yeyote anayewasili haswa wale wanaodai wanatoka Palma, ambako kwa muda mrefu hadi hivi karibuni eneo hilo lilikuwa halina watu," Brigedia Chongo Vidgal aliiambia televisheni inayomilikiwa na serikali Jumapili usiku.

  Alisema "asilimia 95 ya wanamgambo walikuwa Msumbiji.

  Mwaka jana kikundi hicho kiliteka mji wenye kuongoza kwa gesi wa Palma na mji wa bandari wa kimkakati wa Mocímboa da Praia.

  Eneo la Mocímboa da Praia lilitekwa tena wiki iliyopita baada ya kampeni iliyoongozwa na wanajeshi wa Rwanda ambao walipelekwa mkoa huo mwezi uliopita kama sehemu ya makubaliano ya nchi mbili.

  Brigedia Vidgal alisema wanajeshi wa Rwanda walikuwa na vifaa bora na kuongeza kuwa wanajeshi wa Msumbiji "wana hisia kubwa ya uzalendo" na walikuwa wakifanya kazi kwa karibu na wenzao.

  Alisema pia kwamba wanajeshi wa Rwanda walikuwa wepesi kutoa taarifa kuhusu ujumbe huo, ikiwemo kushirikishana picha za wanajeshi kwasababu walikuwa na waandishi wa habari ndani ya jeshi.

  "Sisi pia tuko tunakaribisha waandishi wa habari wa kitaifa kufuata mfano huo," alisema.

  Nchi wanachama katika kambi ya ukanda wa kusini mwa Afrika, Sadc, pia wamejiunga na juhudi za kupambana na wanamgambo wa Kiislam kaskazini mwa Msumbiji.

  Zaidi ya watu 3,000 wameuawa huku wengine 820,000 wakitoroka makazi yao tangu kuanza kwa uasi huko Cabo Delgado mnamo mwaka 2017.