Wakimbizi

 1. Kenya kufunga kambi za Kakuma, Dadaab kufikia Juni 2022

  kambi

  Kenya imethibitisha kuwasiliana rasmi na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR na kutaarifu kuwa itafunga kambi za wakimbizi ya Dadaab na Kakuma ifikapo Juni 30, 2022.

  Waziri wa mambo ya nje wa nchini Kenya bwana Fred Matiangí ametangaza hayo baada ya kufanya mkutano na Filippo Grandi, mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia wakimbizi.

  Dkt. Matiangí amesema kuwa timu ya maafisa wa serikali ya Kenya na Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa watafuatilia mchakato huo uliopangiwa kuanza Mei, 5, 2022.

  Mchakato wa sasa hivi unajumuisha kurejea katika nchi zao kwa hiari au kutoa kibali cha kufanyakazi au cha makazi bila malipo kwa wakimbizi kutoka jamii ya Afrika Mashariki.

  Wakati huo huo, Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limefurahishwa na mpango wa kupitiwa tena kwa mpango wa kufunga kambi hizo za wakimbizi.

  ‘’Sio kambi za kudumu za wakimbizi au kufungwa kwa haraka kwa kambi hizo au kukiuka kanuni ya kimataifa inayokataza nchi inayopokea wakimbizi kuwarejesha nchini mwao ambako wanaweza kuwa katika hatari ni suluhisho ya hili’’, UN imesema.

  Katika taarifa iliyotolewa na shirika hilo, imesema kuwa inaamini serikali ya Kenya na shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa katika kubaini machaguo mengine ya kuwahifadhi au kurejea kwa hiari kwa wanaotaka kwa namna heshima.

  Mnamo mwezi Machi, serikali ya Kenya ilikuwa imeipatia UN makataa ya mwisho ya kutafuta njia kwasababu inataka kufunga kambi hizo mbili ambazo ni makazi kwa wakimbizi 400,000.

  Muda mfupi baadae, Shirika la Amnesty International likajibu kwa kusema kuwa hatua ya kufungwa kwa kambi za Dadaab na Kakuma bila mpangilio unaoheshimu haki za wakimbizi, kutasababisha janga la kibinadamu wakati tayari dunia inakumbana na janga la virusi vya corona.

  Kenya imekuwa ikitoa makazi kwa wakambizi kwa zaidi ya miaka 30 na sasa hivi serikali inasema uwezo wake kuendelea kuwatunza hata kwa kuzingatia viwango vya chini kabisa vya kibinadamu vinavyokubalika imekuwa changamoto kwa nchi hiyo kuvifikia.

  Katibu Mkuu nchini Kenya Karanja Kibicho, aliongeza kuwa uamuzi wake wa kufunga kambi za Dadaab na Kakuma kufikia Juni 30, 2022 ‘ni kwa maslahi ya raia wa nchi yake’.

 2. Marekani yahofia 'kufungwa' kwa kambi za wakimbizi Kenya

  Marekani imeelezea wasi wasi wake kuhusu uwezekano wa kufungwa kwa kwa kambi za wakimbi za Dadaab na Kakuma nchini Kenya.

  Kupitia Waziri wake wa mambo ya nje Anthony Blinken, utawala wa Rais Joe Biden siku ya Alhamisi uliangazia suala lakufungwa kwa kambi hizo mbili.

  Utawala wa Biden inataka kujua hali ya kuregeshwa kwa wakimbizi katika mataifa yao.

  Hii inafuatia mkutano kati ya katibu wa katika Wizara ya Mamboya Nje wa Kenya Macharia Kamau na Derek Chollet ambaye ni mshauri wa sera wa ngazi ya juu wa Waziri wa Mmbo ya ya nej wa Marekani Anthony Blinken.

  Akijibu swali hilo Macharia, hatahivyo, alisema kufungwa kwa kambi hizo mbili za wakimbizi ni swala ambalo limekuwepo tangu mwaka 2016.

  Uchunguzi huo unakuja wakati Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Fred Matiangi na mwenzake wa Masuala ya Kigeni Raychelle Omamo walifanya mkutano na ujumbe wa washirika 25 wa maendeleo mjini Nairobi kujadili suala hilo.

  Washirika has wa kimaendeleo ni pamoja na Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, na wawakilishi wa Shirika la Fedha Duniani (IMF).

 3. Kenya yaagiza kufungwa kwa kambi kubwa ya wakimbizi

  Kambi ya Dadaab
  Image caption: Kambi ya Dadaab

  Kenya imeagiza kufungwa kwa kambi kubwa nchini humo na kutoa siku 14 kwa Umoja wa Mataifa kutatua njia ya kukabiliana na hatua hiyo.

  Karibu nusu milioni ya wakimbizi sasa hivi wanaishi katika kambi za wakimbizi za Dadaab na Kakuma, wengi wao wakiwa kutoka Kusini mwa Sudan na Somalia, nchi ambazo bado haziko thabiti.

  Kenya iliwahi kutishia kufunga kambi hizo siku za nyuma. Lakini leo hii, Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiangí ameliambia shirika la Umoja wa Mataifa kwamba hakuna tena nafasi ya kufanya majadiliano.

  Bwana Matiangí inasemekana kwamba amerejelea vitisho vya mashambulizi ya kigaidi kutoka kambini na pia ametaja uhusiano wa kidiplomasia ambao umezorota kati yake na Somalia.

  Kambi ya Daadab

  Zaidi ya nusu ya wakimbizi nchini Kenya 500,000 ni kutoka Somalia.

  Shirika la Wakambizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) limesema kuwa muda uliotolewa ni mchache mno na kuonya kwamba uamuzi huo huenda ukaathiri ulinzi wa wakimbizi nchini Kenya, hasa ukizingatia janga la virusi vya corona.

  Kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya ni makazi kwa karibu wakimbizi 218,000 wengi wao wakiwa raia wa Somali, huku kambi ya wakimbizi ya Kakuma ikiwahifadhi wakimbizi takriban 200,000 waliosajiliwa wengi wao wakiwa kutoka nchi ya Sudan Kusini iliyoathirika na vita.

 4. Ethiopia yapanga kufunga kambi za wakimbizi Tigray

  Mapigano yalitokea katika eneo Tigray Novemba mwaka jana.

  Ethiopia inapanga kufunga kambi mbili za wakimbizi zilizopio kaskazini mwa jimbo la Tigray ambalo lilikumbwa na vita kati ya waliokuwa watawala (TPLF) na serikali kuu, kwa mujibu wa shirika la wakimbizi nchini humo.

  Akizungumza na wanahabari Jumanne, mkuu wa Shirika la Wakimbizi na Wanaorejea nchini Ethiopia, Tesfaye Gobezay, amesema ukaribu na mipaka ya Eritrea na hali mbaya ya kijiographia ndizo sababu zilizopeekea kufungwa kwa kambi hizo.

  Karibu wakimbizi 100,000 kutoka Eritrea walikuwa wanaishi kambini huko Tigray kabla ya kuanza kwa mapigano mapema mwezi Novemba.

  Kambi mbili - Shimbela na Hitsats – ambazo zilikuwa na zaidi ya wakimbizi 20,000 hazijaweza kufikiwa kwa ajili ya kupewa misaada siku za hivi karibuni.

  Bwana Tesfaye aliongeza kuwa wakimbizi watapelekwa katika kambi zingine au kurejeshwa wenye jamii.

  Hivi karibuni, shirika la UN lilisema kwamba karibu wakimbizi 20,000 wa Eritrea hawajulikani walipo.

  Kulingana na Bwana Tesfaye kumekuwa na majaribio ya awali ya kufunga kambi za Hitsats, lakini juhudi hizo zikashindikana kwasababu chama cha Tigray People’s Liberation Front (TPLF) kilipinga mpango huo na pia janga la corona likachangia.

  “Kulikuwa na mapigano haswa katika kambi hizo” na wakimbizi “walijikuta katika njia panda”,Bwana Tesfaye alisema.

  Hata hivyo uchunguzi zaidi unahitajika kubaini taarifa za kina na ikiwa kuna waliopoteza maisha yao.

 5. Wafungwa 1,789 wa Ethiopia walioko Tanzania kurejeshwa kwao

  Eagan Salla

  BBC Swahili, Dar es Salaam

  K
  Image caption: Rais wa Ethiopia akipiga ngoma mara baada ya kuwasili mjini Chato, Tanzania ambapo alipokelewa na mwenyeji wake rais wa Tanzania.

  Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ameridhia kuwarejesha kwao wafungwa 1789 raia wa Ethiopia waliko kwenye magereza mbalimbali nchini Tanzania wakituhumiwa kuingia nchini kinyume na sheria

  Tanzania imeitaka Ethiopia kufanya taratibu za kuwarejesha nyumbani wakalitumikie na kulijenga taifa lao

  Maamuzi haya yametolewa katika mazungumzo ya kuhitimisha ziara ya siku moja ya rais wa Ethiopia Sahle-Work Zewde ambaye aliwasilia kwenye uwanja wa ndege wa Chato na kupokelewa na mwenyeji wake rais Magufuli na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana kwa takribani saa tatu kabla ya kujitokeza tena hadharani.

  Mataifa haya mawili pia yameazimia kushirikia kwenye biashara ya wanyama na mazao yatokanayo na wanyama kwani Ethiopia imepiga hatua zaidi katika sekta hiyo, hivyo Tanzania itajifunza na kuweza kunufaika katika ushirikiano huo.

  Rais wa Ethiopia Salhe Zedwe alieleza kufurahi kurejea Tanzania na kwamba wamekubaliana na raisi Magufuli kuwa Kiswahili kianze kufundishwa Chuo kikuu cha Adis Ababa huko Ethiopia, Rais Zewde anasema maneno ya kwanza ya Kiswahili aliyojifunza ni “Acha kelele mtoto amelala”

  Tanzania na Ethiopia zimekuwa na mahusiano ya kihistoria na katika kudumisha uhusiano huo Ethiopia imeahidi kuipatia tena Tanzania eneo la Kujenga ubalozi wake baada ya eneo la awali kuchuliwa na serikali kutokana na kutokuendelezwa na serikali ya Tanzania.

 6. Human Rights Watch: Wakimbizi wa Burundi 'wateswa' Tanzania

  Tanzania inatoa hifadhi kwa maelfu ya wakimbizi kutoka Burundi katika kambi zilizo karibu Na mpaka

  Shirika la Human Rights Watch (HRW) limeishutumu Tanzania kwa ‘kuwatesa’ wakimbizi 18 wa Burundi tangu mwaka jana.

  Katika taarifa hiyo, shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu, limesema polisi nchini Tanzania limewakamata na kuwashikilia kiholela wakimbizi 11 wa Burundi kwa wiki kadhaa na kuwazuia katika mazingira mabovu kwenye kituo cha polisi cha Kibondo, mkoani Kigoma.

  Ripoti hiyo pia inaituhumu serikali ya Tanzania kwa kuwarejesha kwa lazima wakimbizi wanane (kati ya 11) nchini Burundi mwezi Agosti mwaka huu. HRW inadai kuwa wanane hao sasa wapo kizuizini nchini Burundi bila kufunguliwa mashtaka. Wakimbizi watatu waliosalia wameachiwa huru nchini Tanzania, ripoti hiyo inasema.

  Wakimbizi saba waliokuwa wanatafuta hifadhi walikamatwa na hawajulikana walipo tangu Januari mwaka huu, HRW imesema.

  “Serikali ya Tanzania inastahili kuchunguza kwa haraka madai kuwa raia wa Burundi wametekwa nyara, kuteswa, wamekamatwa na kukabidhiwa kinyume cha sheria kwa serikali ya Burundi na kuhakikisha walihusika wamechukuliwa hatua,” shirika hilo limesema.

  Serikali ya Tanzania haijazungumzia ripoti hiyo, na juhudi za BBC kupata malelezo ya mwakilishi wa serikali bado hazijafua dafu.

  Raia wa Burundi zaidi ya 150,000 wanaishi katika kambi za wakimbizi nchini Tanzania, wengi wao wakiwa wametoroka machafuko Burundi baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kuamua kugombea urais kwa muhula wa tatu mwaka 2015 hatua iliyozua utata.

  Aidha, shirika la HRW, limesema bado halijapokea taarifa zozote kutoka Tanzania baada ya kutuma barua likitafuta majibu kuhusu uchunguzi wa madai hayo.